Zitto Sitogombea Urais wala Ubunge 2015

Zitto Sitogombea Urais wala Ubunge 2015


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema hafikirii kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho wala ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Alisema mwaka 2015, ndio mwaka wa mwisho kujihusisha na siasa ambapo dhamira yake ni kutafuta chuo ambacho ataweza kufundisha masomo ya uchumi na maliasili.

Bw. Kabwe aliyasema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalumu na gazeti hili siku chache baada ya viongozi 105 kutoka Vyuo Vikuu 30 nchini, kupendekeza majina ya wanasiasa wanaofaa kuwania urais mwaka 2015.

Jina la Bw. Kabwe, lilishika nafasi ya pili katika mchujo huo ambapo Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba, alishika nafasi ya kwanza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwanasiasa aliyeshika nafasi ya tatu katika mchujo huo alikuwa Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam, Bw. John Mnyika (CHADEMA).

"Hiki ni kipindi cha mwisho kwangu kujihusisha na siasa kwani nimechoka nazo, nitatafuta chuo nikafundishe na kama nitakosa ni bora nikalime michikichi... sihitaji urais," alisema.

Katika mkutano wa wanafunzi hao, walisema Bw. Makamba ana sifa zote za kuwa rais wa nchi kamaatagombea nafasi hiyo mwaka 2015 ili aweze kulikomboa Taifa ambalo hivi sasa linakabiliwa na matukio mengi ya uvunjifu wa amani.

Wanafunzi hao walikwenda mbali zaidi na kuyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na vurugu, kutekwa kwa watu wasio na hatia, kufanyiwa vitendo vya ukatili, kumwagiwa tindikali na kupungua kwa mtangamano wa kijamii.

Mwenyekiti wa mkutano huo ambao ulifanyika mkoani Morogoro ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Mbeya, Bw. Theonest Theophil, alisema Bw. Makamba alipata kura 72 ambapo Bw. Kabwe alipata kura 20.

Bw. Theophil alisema sifa za kiongozi wanayemtaka kwanza awe kijana mwenye fikra mpya, atakayeleta matumaini mapya, kuwaunganisha Watanzania, asiyeendekeza siasa za kikanda, mdini na mkabila.

Sifa nyingine ni kiongozi mwadilifu asiye na rekodi ya kutuhumiwa mahali popote kwa vitendo viovu, mtulivu, mwenye busara na anayepima kauli zake.


Source: Majira

go to link download

Comments

Popular posts from this blog

Acer Aspire V3 371 Disassembly Steps

adobe photoshop CS4 extended serial number